2 Corinthians 4

Hazina Ya Mbinguni Katika Vyombo Vya Udongo

1 aKwa hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii kwa rehema za Mungu, hatukati tamaa. 2 bTumekataa mambo ya siri na ya aibu, wala hatufuati njia za udanganyifu, tukichanganya Neno la Mungu na uongo. Kinyume cha hayo, tunadhihirisha kweli waziwazi na kujitambulisha wenyewe kwenye dhamiri ya kila mtu mbele za Mungu. 3 cHata nayo Injili yetu kama imetiwa utaji, ni kwa wale tu wanaopotea. 4 dKwa habari yao, mungu wa dunia hii amepofusha akili za wasioamini, ili wasione nuru ya Injili ya utukufu wa Al-Masihi, aliye sura ya Mungu. 5 eKwa maana hatujihubiri sisi wenyewe ila tunamhubiri Isa Al-Masihi kuwa ni Bwana na sisi ni watumishi wenu kwa ajili ya Isa. 6 fKwa kuwa Mungu, yeye aliyesema, “Nuru na ing’ae gizani,” ameifanya nuru yake ing’ae mioyoni mwetu ili kutupatia nuru ya maarifa ya utukufu wa Mungu katika uso wa Al-Masihi.

7 gLakini tunayo hazina hii katika vyombo vya udongo, ili ijulikane wazi kwamba uwezo huu wa ajabu unatoka kwa Mungu wala si kwetu. 8 hTwataabika kila upande lakini hatuangamizwi; twaona wasiwasi lakini hatukati tamaa; 9 itwateswa lakini hatuachwi; twatupwa chini lakini hatupondwi. 10 jSiku zote twachukua katika mwili kufa kwake Isa ili kwamba uzima wa Isa uweze kudhihirika katika miili yetu. 11 kKwa maana sisi tulio hai siku zote tumetolewa tufe kwa ajili ya Isa, ili kwamba uzima wake upate kudhihirishwa katika mwili wetu upatikanao na mauti. 12 lHivyo basi, mauti inatenda kazi ndani yetu, bali uzima unatenda kazi ndani yenu.

13 mImeandikwa, “Niliamini, kwa hiyo nimesema.” Kwa roho yule yule wa imani pia tuliamini na hivyo tunasema, 14 nkwa sababu tunajua kwamba yeye aliyemfufua Bwana Isa kutoka kwa wafu, atatufufua sisi pia pamoja na Isa na kutuleta sisi pamoja nanyi mbele zake. 15 oHaya yote ni kwa faida yenu, ili kwamba neema ile inavyowafikia watu wengi zaidi na zaidi, ipate kusababisha shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu.

16 pKwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 17 qKwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi, 18 rkwa sababu hatuangalii yale yanayoweza kuonekana bali yale yasiyoweza kuonekana. Kwa maana yale yanayoweza kuonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoweza kuonekana ni ya milele.
Copyright information for SwhKC